KUHUSU SHERIA KIGANJANI
Kwa mujibu wa kifungu cha 8 cha Kanuni ya Adhabu (The Penal Code), Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania kutokujua sheria hakuwezi kumwondolea hatia mtuhumiwa. Utaratibu huu hutumika katika mataifa yote pale ambapo shauri linasikilizwa mahakamani au katika vyombo vingine vyenye hadhi ya kimahakama (Quasi-Judicial bodies). Utaratibu huu hutumika katika masuala yote ya kisheria, ikujumuisha pia mashauri ya madai. Kwa hiyo, ni wajibu wa kila mtu katika jamii kujua sheria, angalau zile zinazozunguka maisha yake ya kila siku, ili inapotokea kwamba ameingia katika mgogoro basi ujuzi alionao umsaidie. Hakuna anayehurumiwa kwa kigezo cha kutokujua Sheria.
Kwa bahati mbaya, kutokana na uhaba wa wanasheria katika nchi yetu, na ukweli kwamba wengi kati ya wanasheria wachache waliopo wanafanyia shughuli zao mijini, sehemu kubwa ya Watanzania wamejikuta wakipata huduma hizi kwa gharama kubwa sana, na wakati mwingine kutozipata kabisa kwa namna inayostahili. Inambidi mwananchi mwenye shida ya huduma za kisheria awe na fedha za kugharimia safari, kujikimu njiani, malazi, tahadhari na fedha za kumlipa wakili. Hii ni gharama kubwa.
Kwa kuzingatia kwamba kujua sheria ni haki na wajibu wa kila mwanajamii, na kwa kufahamu kwamba upatikanaji wa elimu ya sheria ni tatizo kwa sehemu kubwa ya jamii ya Watanzania, hususan walio masikini na wale waishio vijijini, MAWAKILI watatu ambao ni wamiliki wa huduma ya SHERIA KIGANJANI wameamua kwa dhati kuanzisha mfumo huu wa upatikanaji wa huduma za kisheria kwa njia ya mtandao, ambayo itashusha gharama za huduma ya sheria kwa zaidi ya 80% (asilimia themanini) ukilinganisha na gharama za sasa.
Huduma hii itawezeshwa na matumizi yanayozidi kuongezeka ya teknolojia ya mawasiliano kwa mtandao (internet) na simu za mkononi.
MALENGO MAKUU YA TOVUTI HII
Miongoni mwa malengo ya tovuti hii ni kama yafuatayo;
- Kuhakikisha kuwa hakuna Mtanzania anayekosa haki yake ya kisheria kwa sababu ya kutokuwa na uelewa na/au uwezo wa kifedha wa kugharimia masuala ya kisheria
- Kuleta mwamko na hamasa kwa Watanzania katika kupata taarifa, maarifa na elimu juu ya sheria kwa njia ya teknolojia ya mawasiliano (TEHAMA)
- Kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwani wananchi watatumia rasilimali zao kwa makini wakizingatia mipaka ya haki na wajibu walio nao kwa mujibu wa Sheria
- Kuwezesha wanawake, Watoto, walemavu na wananchi wengine walio katika makundi maalum kupata fursa sawa na watu wengine katika umilikaji wa rasilimali na vichocheo vingine vya maendeleo katika jamii
- Kurahisisha ufanyikaji wa biashara kwa kutoa elimu ya ujuzi kuhusu mikataba, sheria za ushindani wa kibiashara, namna ya kuanzisha na kuendesha kampuni ama ubia wa kibishara (partnerships), nk.
FAIDA ZA SHERIA KIGANJANI
- Gharama za upatikanaji wa huduma za kisheria Tanzania zitashuka.
- Mrundikano wa mashauri mahakamani utapungua kwani wananchi wenye uelewa wa sheria watakuwa na uwezo wa kutatua migogoro midogomidogo miongoni mwao kwa urahisi.
- Pengo la upungufu wa watoa huduma za ushauri wa kisheria litapungua kwani wananchi wengi watapata huduma hii popote walipo kwa wakati mmoja.
- Madhara-tarajiwa (risks) yatokanayo na kusafiri yatapungua kwani huduma hii itawafuata wananchi pale pale walipo.
- Fursa kwa wananchi kuzungumza na mwanasheria wakati wowote kadiri ya mahitaji na shida zao.